Jinsi ya kupika Pilau ya kuku

Jinsi ya kupika Pilau ya kuku


jinsi ya kupika pilau ya kuku: Habari za leo wapenzi wa blogu yetu hii ya Mapishi ya kiswahili. Leo tunakuletea pishi la chakula kipendwacho na wengi, Pilau ya kuku. Fuatana nami hatua kwa hatua namna ya kupika wali huu.

Jinsi ya kupika pilau ya kuku: Hatua kwa hatua

Mahitaji

  • Mchele wa basmati         kilo 1
  • Kuku                              ½
  • Viazi                               5
  • Vitunguu                          2
  • Thomu iliyosagwa             3 vijiko vya supu
  • Binzari ya pilau nzima       1 Kijiko cha chakula
  • Binzari ya pilau                 1 kijiko cha chai
  • Pilipili manga nzima           ½ kijiko cha chai
  • Karafuu nzima                    10
  • Iliki nzima                          8
  • Mdalasini nzima                 6 vijiti
  • Pilipili mbichi iliyosagwa     3
  • Chumvi                             kiasi
  • Mafuta ya kupikia              ¼ lita

Namna ya kupika pilau- Hatua kwa hatua

  1. Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
  2. Kata kuku vipande upendavyo, safisha kisha chemsha vipande vyako pamoja na chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu na tangawizi.
  3. Kuku akishawiva, mtoe weka kwenye bakuli safi, Bakisha supu katika sufuria.
  4. Tia mafuta kiasi katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi na kuwa ya hudhurungi.
  5. Tia thomu na tangawizi na binzari zote, kisha kaanga tena kidogo.
  6. Tia viazi katika mchanganyiko wako huo, kisha endelea kukaanga kidogo.
  7. Tia vipande vyako vya kuku na supu (iliyobaki wakati wa kupika kuku) katika mchanganyiko wako huo, acha ichemke kidogo kisha tia maji, kisia kutokana na mchele unaotumia.
  8. Mwisho tia mchele koroga uchanganye na vitu vyote acha ichemke kiasi kisha funika na punguza moto mpaka uive (huku ukiugeuzageuza).
  9. Ukishakuwa tayari pakua  kwenye sahani tayari kwa kula.
Pishi la pilau: Dondoo
Chakula hiki kinaweza kutosha mlo wa watu 3-4, unaweza kuongeza au kupunguza vipimo vya mahitaji kulingana na idadi ya walaji. Pilau ya kuku ni vizuri ikiliwa na salad na pilipili. Pia unaweza kushushia pamoja na juisi ya matunda. Natumai umefurahia pishi letu la leo waweza kutoa maoni yako hapo chini kuhusu jinsi ya kupika pilau ya kuku. Akhsanteni